News

KAMATI YA BUNGE YA MIUNDOMBINU YAIPONGEZA UCSAF KUFIKISHA HUDUMA ZA MAWASILIANO KWA WOTE

Posted On: Thursday 12, July 2018

Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Miundombinu imeupongeza Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kwa kufikisha mawasiliano kwa watanzania waishio sehemu mbali mbali nchini ambako hapakuwa na mawasiliano hapo awali na maeneo ambayo hayana mvuto wa kibiashara ambapo makampuni ya simu hayakuvutiwa kuwekeza na kutoa huduma kwa wananchi.

Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu Mhe. Moshi Selemani Kakoso wakati Kamati yake ilipofanya ziara ya kutembelea UCSAF ili kufuatilia utekelezaji wa majukumu yao na kujenga uelewa namna wanavyotekeleza majukumu yao.

Mheshimiwa Kakoso ameipongeza UCSAF kwa kufikisha huduma za mawasiliano kwa kwa wananchi katika maeneo ambayo hapakuwa na mawasiliano kwa kiwango cha asilimia 94 sehemu mbali mbali nchini ambapo sasa wamewawezesha wananchi kuwasiliana na kupata huduma mbalimbali.

Aidha, Kakoso ameitaka UCSAF ijitangaze vya kutosha ili wananchi waelewe na waweke nembo kwenye minara 530 ya mawasiliano iliyojengwa na kampuni za simu za mkononi kwenye kata mbali mbali nchini baada ya kupatiwa ruzuku na Serikali. Ameongeza kuwa, UCSAF imetoa ruzuku na kuziwezesha kampuni kujenga minara ambapo vodacom imejenga minara 189, Shirika la Mawasiliano (143), TIGO (116), Halotel (47) na Zantel (2).

Naye Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Mhandisi Atashasta Nditiye (Mb), akizungumzia kwa niaba ya Serikali amesema kuwa, Serikali imejipanga kuhakikisha kuwa watanzania wanawasiliana kwa kuwa wakiwasiliana na kutumia huduma mbali mbali za mawasiliano, Serikali inapata mapato na kukuza uchumi wa nchi. Pia, ameongeza kuwa Serikali itaongeza minara ya mawasiliano Pemba ili kuendana na hali ya mazingira ya kijiografia ya eneo hilo ili kuhakikisha kuwa wananchi wote wanapata huduma za mawasiliano. Amesema kuwa, Serikali imeongeza fedha kwa UCSAF ili iendelee kujenga minara nchini kwa kuongeza kiwango cha mapato yake kutoka kampuni za simu za mkononi kutoka asilimia 0.3 hadi asilimia 0.9 ya mapato ghafi ya mawasiliano ya kampuni za simu za mkononi.

Aidha, Serikali imedhamiria kuongeza kiwango hicho hadi kufikia asilimia 1 ya mapato ghafi ya mawasiliano ya kampuni za simu za mkononi kwa UCSAF ili iweze kuendelea kujenga minara na kufikisha huduma za mawasiliano kwa wanachi waliosalia kiwango cha asilimia 4 ambao hawana mawasiliano kwenye baadhi ya maeneo mbali mbali nchini.

Wakati akifanya wasilisho lake kwa Kamati hiyo, Mtendaji Mkuu wa UCSAF Mhandisi Peter Ulanga amesema kuwa UCSAF imetumia jumla ya shilingi bilioni 97.8 kufikisha mawasiliano kwa wananchi sehemu mbali mbali nchini ambapo jumla ya kata 530 zimejengwa minara hiyo yenye jumla ya vijiji 2,132 na wakazi milioni 3.6. Ameongeza kuwa, UCSAF imetekeleza miradi mingine ikwemo ya kutoa mafunzo ya TEHAMA kwa waalimu 925 wa shule za mbali mbali nchini katika kipindi cha mwaka 2015/2016 hadi mwaka 2017/2018 ambapo mafunzo hayo yanawawezesha waalimu kufundisha masomo ya TEHAMA na kufanyia matengenezo vifaa vya TEHAMA na kompyuta vinapoharibika shuleni hivyo kupunguza gharama za matengenezo.

Mhandisi Ulanga amefafanua kuwa, tayari UCSAF imeziunganisha shule 255 na huduma ya mtandao wa intaneti, imetoa kompyuta 700, printa 10 na projekta 20 kwenye shule zilizopo maeneo mbali mbali nchini. Pia, UCSAF imetoa mafunzo ya TEHAMA kwa wasichana 448 katika kipindi cha mwaka 2016 hadi 2018 ili kuwaongezea ari na mwamko wa kusoma masomo ya TEHAMA.

Mhandisi Ulanga amewaeleza wajumbe wa Kamati hiyo kuwa, katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2018/2019, UCSAF imejipanga kujenga minara na kufikisha huduma za mawasiliano kwenye kata nyingine 100, kutoa mafunzo ya TEHAMA kwa waalimu 500 na kugawa vifaa vya TEHAMA na kompyuta 700 kwenye shule mbali mbali nchini.