News

KAMATI YA MIUNDOMBINU YATAKA THAMANI YA FEDHA KATIKA MIRADI YA RELI

Posted On: Monday 02, July 2018

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeutaka uongozi wa Kampuni ya Reli (TRC), kuhakikisha fedha zilizotengwa kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya reli zinatumika kwa miradi iliyotengewa ili ikamilike kwa wakati na viwango.

Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Seleman Kakoso, ameyazungumza hayo mwishoni mwa wiki mkoani Kilimanjaro, mara baada ya kukagua maendeleo ya ukarabati wa reli ya kaskazini kuanzia Tanga-Moshi-Arusha, na kusisitiza kuwa reli hiyo nimuhimu sana kwa maendeleo ya uchumi wa Taifa.

“Hakikisheni mnatumia fedha za miradi kwa maeneo husika kwani Serikali imejikita katika kuhakikisha fedha zinazoidhinishwa kwenye miradi zinatumika vizuri bila kubadilishwa matumizi ”, amesisitiza Mhe Kakoso.

Aidha Mhe. Kakoso, amesema kuwa ni wakati sasa kurudisha nguvu kwenye reli ya kati ili kusafirisha mizigo mikubwa na kuufikisha kwa watumiaji kwa wakati na hivyo kunusuru uharibifu wa barabara unaoendelea kujitokeza.

Ameongeza kuwa kazi za ukarabati zinazofanywa zifanyike kwa wakati mmoja sambamba na utoaji wa elimu kwa maeneo yote ya hifadhi ya reli ili kuepusha migogoro inayoweza kutokea kwa wananchi waliovamia maeneo ya reli nchini.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Sekta ya Uchukuzi, Dkt Leonard Chamuriho, amesema kwa sasa Serikali imeamua kuwekeza kwenye uboreshaji wa reli iliyopo na Reli ya Kisasa ya Standard Gauge ambao ujenzi wake unaendelea kwa awamu ya kwanza inayotoka Dar es Salaam mpaka Morogoro na ile awamu ya pili inayoanzia Morogoro mpaka Makutupora, Dodoma.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Bw. Masanja Kadogosa, amewaeleza wajumbe wa Kamati kuwa kazi zinazoendelea ni ukarabati wa njia kuanzia Mombo mpaka Moshi na sehemu ya ukarabati kuanzia Tanga mpaka Mombo umeshakamilika.

Ameongeza kuwa kazi zitakazofuata baada ya kukarabati njia ni kukarabati madaraja yaliyo katika njia hiyo na hatua ya mwisho sasa itakuwa kupitisha treni ya mizigo ili kupima uimara wa reli hiyo kabla haijaanza kutumika kwa treni za abiria.

Kuhusu suala la ajira, Bw. Kadogosa amefafanua kuwa kampuni inafanya ukarabati kwakuwatumia wananchi ambao wanaishi maeneo jirani na reli inapopita na kuahidi kuwaajiri mara ya ukarabati huo kukamilika ili waweze kuitunza reli hiyo.