News

PROFESA MBARAWA AKAGUA MAENDELEO UJENZI WA TAZARA FLY OVER

Posted On: Wednesday 06, June 2018

WaziriI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesema daraja la Tazara ‘Flyover’ linatarajiwa kufunguliwa rasmi Septemba mwaka huu na Rais John Magufuli.

Prof. Mbarawa aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari baada kufanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa daraja hilo la kisasa nchini Tanzania.

Alisema daraja hilo ambalo linapaswa kujengwa kwa miezi 36 linataanza kutumia rasmi mwezi wa Septemba ikiwa ni muda sahihi kulingana na mkataba.

Waziri alisema hadi sasa ujenzi umefikia asilimia 88.82 hivyo kama hakutakuwa na mabadiliko Septemba mwaka huu Rais Magufuli atafungua rasmi na kuanza kutumika.

Alisema hadi kukamilika kwa daraja hilo zaidi ya Sh. Bil 95 zitakuwa zimetumika ikiwa ni fedha kutoka nchini Japani kupitia Shirika la Maendeleo la Japani (JICA).

“Daraja hilo la Tazara ‘Flyover’ linatarajiwa kufunguliwa rasmi Septemba mwaka huu kwani hadi sasa ujenzi umefikia asilimia 88.82 na Rais ndio anatarajiwa kufungua,” alisema Mbarawa.

Alisema mwezi Agosti mwaka huu wataanza kufanya majaribio ya daraja hilo baada ya kazi zote muhimu kukamilika kama inavyotarajiwa.

Waziri Mbarawa alisema hadi sasa mkandarasi Sumotomo Mitsui Construction Co, Ltd ametumia saa Mil. 2.16 ambapo ujenzi umebakia katika maeneo ya kuingilia.

Alisema hadi sasa hakuna ajali ambayo imetokea tangu ujenzi uanze jambo ambalo ni la kupongezwa na kwamba ni moja ya sababu ya mradi kuenda kwa kasi.

Mbarawa alisema kukamilika kwa daraja hilo kutapunguza msongomano na foleni katika eneo hilo la Tazara ambapo wasafiri watatumia dakika zisizozidi 30 kutoka mjini hadi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).

“Kwa sasa ili kufika mjini kwa njia ya Nyerere unatumia zaidi ya saa mbili ila kukamilika kwa mradi huu haitazidi nusu saa,” alisema.

Mbarawa alisema serikali kupitia wizara yake wanajipanga kujenga madaraja mengine eneo la Chang’ombe, Kurasini, Mwenge, Ubungo ‘Interchange’ na Salender lengo likiwa ni mkakati wa kupunguza msongamano na foleni jijini Dar es Salaam.

Aidha, alisema Serikali katika bajeti yake 2018/19 imetenga Sh. Bil 20 ili kujenga barabara za kufungia jiji ambalo linakabiliwa na msongamano.

Kwa upande wake Balozi wa Japani nchini Tanzania, Masaharu Yoshida alisema anajisikia furaha kuona mradi huo unaenda kwa kasi ambayo ilitarajiwa hali ambayo itapunguza msongamano wa mgari katika eneo hilo.

Yoshida alisema serikali ya Japani imedhamiria kusaidia Tanzania katika miradi ya maendeleo kwa maslahi ya nchi.

Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (Tanroads), mkoa wa Dar es Salaam Mhandisi Julius Ndyamukama, alisema changamoto zilizojitokeza katika ujenzi wa daraja hilo ni uongozaji wa magari lakini walifanikiwa kuzikabili.

Ujenzi wa daraja la Tazara lilikuwa pendekezo la Rais mstaafu wa awamu ya nne Jakaya Kikwete katika ahadi zake ambapo mkataba wa ujenzi ulisainiwa Septemba 2015.