News

RAIS MAGUFULI AWEKA JIWE LA MSINGI UPANUZI BARABARA YA MOROGORO

Posted On: Wednesday 19, December 2018

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.John Pombe Magufuli, amemtaka mkandarasi wa kampuni ya Estim construction Limited iliyopata zabuni ya kujenga upanuzi wa barabara ya Morogoro kuanzia Kimara - Kibaha (km 19.2), kuhakikisha anakamilisha kazi hiyo mapema.

Ametoa agizo hilo leo mkoani Dar es Salaam katika sherehe za uwekaji wa jiwe la msingi la upanuzi wa barabara hiyo ambapo amesema ikiwezekana mkandarasi huyo afanye kazi usiku na mchana ili kufanikisha kazi hiyo kwa muda aliopangiwa.


Amewataka wananchi wa Kimara mkoani Dar es Salaam kuachana na dhana ya kulipwa fidia kwani Serikali haitalipa fidia na kwamba haijamdhulumu mwananchi yeyote isipokuwa inatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria.


"Ukisogelea barabara hasa hifadhi ya barabara ni kosa kisheria, sheria ni msumeno na watanzania tujifunze kuheshimu sheria" ameongeza Rais Magufuli

Rais Magufuli amefafanua kuwa Sheria ya barabara ilianza tangu mwaka 1932 na baadae ilikuja kufanyiwa marekebisho mwaka 1967 ambapo ilizungumza wazi kuhusu upana wa mita za barabara na hifadhi yake.

"Sheria ya barabara inasema kutoka katika sanamu la Askari lililopo Posta jijini Dar es Salaam hadi Ubungo upana wa barabara ni mita 22 kila upande, kutoka Ubungo hadi Kimara Stop Over upana wa barabara utakuwa mita 90 kila upande na kutoka Stop Over hadi Kimara Tamko upana wa barabara itakuwa mita 121 kila upande au futi 400 .............", amesema Rais Magufuli.


Aidha, ameongeza kuwa upanuzi wa barabara hiyo kutoka njia mbili hadi kuwa njia nane ni moja ya utekelezaji wa uboreshaji wa miundombinu ili kuenda sambamba na ongezeko la idadi ya watu.

Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, amesema kuwa ujenzi wa barabara hiyo ni muhimu kwa jiji la Dar es Salaam ambapo inakadiriwa kuwa magari zaidi ya 50000 hutumia barabara hiyo kwa siku, hivyo upanuzi wake ni muhimu katika maendeleo ya ukuaji wa uchumi wa nchi.


"Barabara hii ni lango kuu la usafiri kati ya mkoa huu na mikoa mingine pamoja na nchi jirani kama vile Zambia, Malawi, Burundi na nyinginezo, kwa sababu ya umuhimu wake imepewa namba moja na kuitwa jina la 'Tanzania One' " , amesema Waziri Kamwelwe.
Naye, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Mhandisi Patrick Mfugale, amesema kuwa barabara hiyo inajengwa kwa viwango vilivyo bora ili kuhimili uzito wa magari yanayopita katika barabara hiyo.


Ameongeza kuwa mradi huu unahusisha ujenzi wa madaraja sita katika mto Kibamba, Kiluvya na Mpiji na Makalvati 36 pamoja na kujenga barabara ya juu katika eneo la Kibamba CCM kwenye makutano ya barabara inayotokea Bunju na barabara ya kwenda hospitali ya Mloganzila.


Mradi huu ambao umeanza kujengwa mwezi Julai mwaka huu, unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 30 na kugharimu kiasi cha shilingi Bilioni 141.56.