News

TCAA YASHAURIWA KUWEKEZA KWENYE WATAALAMU WA NDANI

Posted On: Monday 09, July 2018

Kamati ya kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeishauri Mamlaka ya Usafiri wa Anga Nchini (TCAA) kuwekeza kwenye rasilimali watu ili kuongeza tija kwa wataalam wa ndani mara baada mradi wa ujenzi wa rada nne kukamilika.

Akizungumza mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa rada katika kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Mwl. Julius Nyerere (JNIA), Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Selemani Kakoso, amesema kuwawezesha wataalam wa ndani kutawajengea uwezo wa kwenda na kasi ya teknolojia kwenye uongozaji ndege.

“Mradi huu utatumia fedha nyingi hivyo ni vyema kuzingatia wataalam wa ndani kupata elimu ya rada hizi ili mradi ukikamilika wasimamie vyema na si watalaam kutoka nje ya nchi”, amesisitiza Mhe. Kakoso.

Mhe. Kakoso, amesema kuwa Kamati imeridhishwa na kasi ya ujenzi wa rada unaoendelea na kuwataka mradi ukamilike kwa kuzingatia viwango vilivyowekwa kwenye mkataba.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhe. Elias Kwandikwa, amesema uboreshaji wa Viwanja vya ndege mbalimbali nchini unafanywa kwa pamoja na ufufuaji wa Shirika la Ndege ambapo mpaka sasa Serikali imeshanunua ndege sita.

NayeMkurugenzi Mkuu wa TCAA, Hamza Johari ameihakikishia Kamati kuwa mradi huo utakamilika kwa wakati na kwa viwango na kusema kuwa tayari kuna wataalam zaidi ya 20 ambao watapata mafunzo ili kuongoza rada hizo mara baada ya mradi kukamilika.

“Nawahakikishi Waheshimiwa Wabunge kuwa mradi huu utakamilika kwani hakuna changamoto yoyote kifedha na kiutalaam kwani fedha zipo na wataalam wapo, hivyo hatuna sababu za kuchelewesha mradi” amesema Johari.

Katika hatua nyingine Kamati imetembelea Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) na kuipongeza Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Nchini (TAA), kwa kununua gari jipya la Zimamoto ambalo litatumika katika kiwanja hicho na kukifanya kuendelea kuwa salama kwa kuzingatia viwango vya Kimataifa vya Usafiri wa Anga.