News

TRC YATAKIWA KULIPA FIDIA WANANCHI WALIOPISHA UJENZI WA RELI YA KISASA

Posted On: Monday 09, July 2018

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeitaka Kampuni ya Reli Tanzania (TRC) kulipa fidia mapema kwa wananchi wote wanaopitiwa na ujenzi wa reli ya kisasa ya Standard Gauge ili kuepuka changamoto zinazoweza kujitokeza na uhujumu wa mradi.

Akizungumza mara baada ya kukagua maendeleo ya mradi huo Mkoani Pwani, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Selemani Kakoso, amesema kuwa utekelezaji wa mradi huo lazima uende pamoja na utoaji elimu kwa wananchi wanaopitiwa na mradi huo ili waone thamani na umuhimu wa kulinda miundombinu hiyo.

“Hakikisheni wananchi wanaopitiwa na mradi huu wanalipwa fidia zao mapema pia elimu itolewe kwa wananchi hao ili waweze kuilinda miundombinu hii itakapokamilika sababu Serikali inatumia fedha nyingi kwenye utekelezaji wa mradi huu”, amesema Mhe. Kakoso.

Mwenyekiti Kakoso, amesema Kampuni ya TRC inatakiwa kutengeneza mpango kazi wa muda wa kati na mrefu ili kuweza kujiendesha kibishara kwani lengo la kampuni hiyo kuanzishwa ni kujiendesha kibiashara bila kutegemea fedha za Serikali.

Aidha, ameitaka TRC kuhakikisha wanawajengea uwezo wahandisi wa kampuni ili waweze kusimamia kikamilifu mradi huo mara baada ya mradi kukamilika.

Naye Naibu Waziri, Elias Kwandikwa, amesema Serikali itaendelea kuwekeza kwenye miundombinu ili kuchochea uchumi wa viwanda na hatimaye kuharakisha maendeleo yatakayokuza pato la nchi na wananchi kwa ujumla.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa, amesema kampuni imeweka wahandisi wake kwenye eneo la mradi ili kuwajengea uwezo wa kusimamia mradi mzima baada ya kukamilika.

Mkurugenzi huyo, ameongeza kuwa pamoja na utekelezaji wa mradi huo Kampuni ya Yapi Markezi inakamilisha ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza mataruma sehemu ya Soga ambacho kitaanza uzalishaji hivi karibuni.

Kamati ya Kudumu ya Bunge imemaliza ziara yake ya mafunzo ya siku tano katika miradi ya Sekta ya Uchukuzi kwa kutembelea mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa ya SGR.