News

WAZIRI MBARAWA AWATAKA TPA KUSIMAMIA MRADI SAA 24

Posted On: Thursday 07, June 2018

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), kuhakikisha wahandisi wa Mamlaka wanasimamia mradi wa upanuzi wa bandari unaojulikana kama “Dar es Salaam Gateway Project(DMGP) kwa saa 24 ili mradi huo ukamilike kwa wakati na kwa viwango.


Waziri Prof. Mbarawa ametoa agizo hilo leo alipokagua maendeleo ya mradi huo ambao kukamilika kwake kutaongeza pato la mamlaka na kuinua uchumi wa Tanzania pamoja na nchi jirani na kusisitiza mradi huo ni muhimu sana kwa ufanisi wa bandari ya Tanzania.

"TPA lazima muhakikishe wahandisi wa Mamlaka wanakuwa eneo la mradi saa 24 kuanzia sasa maana mradi huu ni mkubwa na unahitaji wataalam wetu kujifunza na kuusimamia mara baada ya kukamilika kwake", amesema Waziri Prof Mbarawa.

Ameeleza kuwa baada ya kuanza ujenzi wa mradi huo kumetokea changamoto ya eneo la mradi kuwa na mchanga laini na kusema kuwa changamoto hiyo haitasababisha mradi kuchelewa kukamilika.

Aidha, Waziri Prof. Mbarawa ameiagiza TPA kuhakikisha ujenzi huo hauathiri shughuli za kupakia na kupakua mizigo zinazoendelea bandarini hapo ili nchi isipoteze pato kwa utekelezaji huo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi Deusdedit Kakoko, amemuhakikishia Waziri Prof. Mbarawa, kuwa Mamlaka imejipanga na inasimamia mradi huo kwa karibu ili ukamilike kwa kuzingatia viwango na muda uliokubaliwa.

Mhandisi Kakoko, ameeleza kuwa ili kuongeza idadi ya wataalam Mamlaka imeomba wahandisi kwenye vyuo vya Uhandisi nchini ili kuwapa fursa ya kujifunza kwa vitendo kupitia mradi huo mkubwa nchini.

"Mradi huu ni moja kati ya miradi mikubwa ya bandari hivyo utekelezaji wake utatoa fursa kwa wahandisi kuja kujifunza kwa vitendo sababu tayari nimeshaandikiwa baadhi ya vyuo vinavyotoa kozi za uhandisi hapa nchini ili na wao waje kujifunza kwa vitendo kupitia mradi huu mkubwa.

Mradi wa upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam unahusisha uboreshaji wa Gati namba 1 mpaka 7, ujenzi wa gati ya kupakia na kupakua magari na upanuzi wa lango la kuingilia bandarini na mradi utagharimu kiasi cha shilingi zaidi ya bilioni 300 na unatarajiwa kukamilika miezi 36.