News

WIZARA YATOA MAFUNZO YA UKANDARASI KWA WANAWAKE

Posted On: Friday 31, May 2019

Wizara ya Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano imetoa mafunzo ya ukandarasi wa barabara kwa wanawake wa mikoa mitano kwa lengo la kuongeza ufanisi wa kazi za ujenzi na matengenezo ya barabara katika kuelekea uchumi wa viwanda hapa nchini.

Wanawake waliopata fursa ya kupata mafunzo hayo ni kutoka mikoa ya Kigoma, Arusha, Pwani, Njombe na Morogoro ambapo wito umetolewa kwa wanawake kuchangamkia fursa hiyo ili kukabiliana na wimbi la umasikini.

Akifungua mafunzo hayo mwanzoni mwa wiki Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Morogoro Mhandisi Godwin Andalwisye, amesema Wizara imeamua kutoa mafunzo hayo kwa wanawake ili kuwajengea uwezo wa matumizi ya teknolojia ya nguvu kazi katika ujenzi na matengenezo ya barabara.

“Sekta ya ujenzi imekuwa ikitekeleza sera mbalimbali kwa lengo la kuongeza ushiriki wa wanawake katika kazi ya ujenzi na matengenezo ya barabara nchini hivyo mafunzo haya yatasaidia kuwajengea uwezo”, amesisitiza Mhandisi Andalwisye.

Ameongeza kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwani yatasaidia kuendela kujengea uwezo katika ukarabati na matengenezo ya barabara hali itakayasaidia kuongeza wakandarasi wanawake na kukuza sekta ya uchumi kwa ujumla.

Aidha, Mhandisi Andalwisye amefafanua kuwa serikali kupitia Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano imelenga kuwawezesha makandarasi wanawake ili waweze kuingia katika ushindani wa kuomba kazi na kuwawezezesha kujua namna ya kujaza nyaraka za zabuni na utekelezajiwa miradi ya barabara kwa kuzingatia mikataba.

"Wizara ina amini kitendo cha ushirikishwaji wa wanawake katika suala zima la ukandarasi na matengenezo ya barabara kitaleta tija katika sekta ya ujenzi hapa nchini", amesema Mhandisi Andalwisye.

Kwa upande wake Mratibu wa kitengo cha mafunzo hayo kutoka Sekta ya Ujenzi, Mhandisi Liberatha Aloyce,amesema kuwa mafunzo hayo yatafanyika zaidi ya wiki moja ambapo yatatoa fursa kwa wanawake kujifunza mambo mbalimbali yanayohusu teknolojia ya barabara.

Mhandisi Liberatha ameendelea kueleza kuwa mara baada ya mafunzo hayo ya nadharia na vitendo kufanyika washiriki watakwenda kufanya kazi kwa vitendo ambapo aliwataka wanawake hao kufanya kazi kwa kuzingatia waledi kwa manufaa ya Taifa zima kwa ujumla.

Mafunzo ya wanawake makandarasi hapa nchini yanaratibiwa na Kitengo cha Ushirikishwaji wa Wananwake kilichopo Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano yakiwa na lengo kuu la kuwawezesha makandarasi wanawake ili waweze kusajili vikundi au makampuni yatakayokuwa chini ya Bodi ya Usajili wa Makandarasi(CRB) na kuweza kutekeleza kazi zao kisheria na kwa waledi.